Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, ametembelea eneo la daraja la Mzinga Mbagala wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, kukagua maandalizi ya ujenzi wa miradi mikubwa inayolenga kupunguza msongamano wa magari katika eneo hilo.
Miradi hiyo ni upanuzi wa barabara kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe yenye urefu wa Kilometa 3.8 kwa kiwango cha lami na ujenzi wa daraja jipya la Mzinga.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Ulega amesema miradi hii ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutatua changamoto za msongamano jijini Dar es Salaam.
“Tumepokea maelekezo mahususi kutoka kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha msongamano mkubwa unaoathiri watumiaji wa barabara katika eneo hili unakwisha. Watanzania wanapoteza hadi masaa matatu kwenye foleni. Tunakwenda kujenga barabara sita, mbili kati ya hizo zitakuwa maalum kwa mabasi yaendayo haraka (BRT), na daraja la Mzinga litapanuliwa kuwa na urefu wa mita 60,” alisema Ulega.
Ameongeza kuwa Serikali itahakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vya juu kwa kuwapa kazi wakandarasi wenye uwezo mkubwa.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa daraja la Mzinga unafadhiliwa na Benki ya Dunia (World Bank), ambapo benki hiyo imetoa takribani dola za Kimarekani milioni 70 kupitia Mpango wa Dharura (Crisis Response Window).
“Manunuzi ya miradi hii yanatarajiwa kukamilika Januari 31, 2025, na mkandarasi atapatikana Februari 2025. Ujenzi wa barabara ya kilomita 3.8 na daraja la Mzinga utaanza mara moja” alisema Besta.
Daraja la sasa la Mzinga lenye urefu wa mita 45 na upana wa mita 9 litaongezewa njia mbili kila upande na sehemu ya mabasi yaendayo haraka, huku barabara ya Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe ikipanuliwa kuwa na njia sita pamoja na maeneo ya watembea kwa miguu na waendesha pikipiki.
Mhandisi John Mkumbo ambaye ni Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, amesema fidia ya shilingi bilioni 12.6 tayari inalipwa kwa wananchi wanaopisha mradi huo.
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Mbagala, Abdallah Chaurembo, ameipongeza Serikali kwa juhudi zake na kuomba uharakishaji wa mchakato wa kumpata mkandarasi ili kazi zianze mwezi Machi 2025.
“Barabara hii ni lango kuu kwa watu wanaotoka na kwenda mikoa ya Kusini. Tumeshuhudia fidia ikilipwa kwa wananchi, na sasa tunaomba kazi ianze haraka,” alisema Chaurembo.
Miradi hii inatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa msongamano katika eneo la Mzinga na Mbagala, huku ikitoa matumaini makubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam na watumiaji wa barabara hiyo.