Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) imekutana na wananchi wa eneo la Msakuzi kwa Lubaba, Kata ya Mbezi, Wilaya ya Ubungo kwa lengo la kufahamu mipango na maendeleo ya miradi ya uboreshaji huduma ya maji katika eneo hilo.
Akizungumza katika mkutano wa ulioitishwa na wananchi hao, Meneja wa DAWASA Ubungo, Mhandisi Edson Robert amesema kuwa mradi wa kusambaza maji katika eneo la Msakuzi kwa sasa unaendelea na tayari mabomba ya inchi 6 yameshafika katika eneo la Serikali ya Mtaa Lubaba kwa ajili ya ulazaji na hatua inayofuata ni ulazaji wa mabomba madogo madogo katika mitaa hiyo ili Wananchi waanze kunufaika na huduma.
“Mpaka sasa mradi umeshafika katika mtaa wetu wa Lubaba na hatua inayofuata sasa ni ulazaji wa mabomba madogo ya kuanzia inchi 3 hadi 2 ili kusambaza maji mtaani na kwa mwananchi mmoja mmoja.” Amesema Mhandishi Robert.
Naye mmoja wa wananchi wa Mtaa wa Kwa Lubaba Makombora Mohammed Issa amesema kuwa kwa kipindi kirefu wamekuwa na changamoto ya maji lakini sasa matumaini yameanza kurejea baada ya kupata maneno ya matumaini kutoka kwa Mamlaya husika.
“Tunashukuru DAWASA kwa kuitikia wito wa kuja kutusikiliza na kutupa majibu ya hoja zetu za maji, tunategemea maji yatatufikia mapema ili wananchi tuepukane na shida ya maji katika mtaa wetu.” Amesema Issa.
DAWASA kwa kushirikiana na wananchi wa Msakuzi Kwa Lubaba wameunda timu ndogo ya kufuatilia umaliziaji wa mradi kwa sehemu iliyobaki ya ulazaji mabomba kwa ajili kusambaza kwa wananchi.