
NA MWANDISHI WETU
WAKATI Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
na Malawi (MDF), Jenerali Jacob Mkunda na Jenerali Vicent Nundwe wakiipongeza
Benki ya NMB kwa udhamini mnono na endelevu wa Mashindano ya Gofu ya NMB
CDF Trophy, benki hiyo imezihakikishia taasisi hizo kuwa itaendelea kudhamini
mashindano hayo, na kuwa siri ya hilo ni mashirikiano bora yaliyopo baina ya NMB na
JWTZ.
NMB ilidhamini mashindano hayo ya Gofu ya Mkuu wa Majeshi (CDF Trophy 2023) kwa
kiasi cha Sh. Mil. 30, kufanikisha kuwaleta pamoja wakali wa gofu 228 waliochuana kwa
siku tatu kwenye Viwanja vya Gofu Lugalo, kuadhimisha Miaka 59 ya kuzaliwa kwa
JWTZ Septemba Mosi 1964, washiriki wakitokea JWTZ, MDF na raia kutoka mataifa
haya mawili jirani.
Wakizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo na kugawa zawadi kwa washindi,
Jenerali Mkunda na Jenerali Nundwe, walikiri kutambua thamani kubwa ya mchango wa
NMB na wadhamini wenza katika kufanikisha michuano hiyo, wanayoitumia kama
jukwaa huru la kuimarisha afya za washiriki na kubadilishana mawazo ya kujiimarisha
Kidiplomasia baina ya Majeshi ya Tanzania na Malawi.
Jenerali Mkunda, aliipongeza Klabu ya Gofu Lugalo (TPDF Lugalo Golf Club) kwa
ubunifu wa shindano hilo, lakini akasema wazo hilo la Brigedia Jenerali Mstaafu Michael
Luwongo (ambaye ni Mwenyekiti wa Gofu Lugalo), lisingewezekana kirahisi kama sio
nguvu na sapoti kubwa ya udhamini mnono wa NMB na kwamba ana furaha baada ya
kuhakikishiwa udhamini endelevu kutoka kwa benki hiyo.
“Pongezi za dhati kwako Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo kwa ubunifu wako
huu wa CDF Trophy, uliowezesha kutukusanya pamoja JWTZ, MDF na washiriki wa
kiraia kwa miaka yote hiyo, ikiwemo miaka nane ya udhamini wa NMB, ambao kama si
wao, shindano hili lisingekuwa kubwa na lenye mvuto kama lilivyo.
“Zilikuwa siku nzuri, zilizotuweka pamoja na kutupa muda wa kushirikiana, kujadiliana
masuala mbalimbali ya Kimichezo na Kidiplomasia, tunatambua na kuthamini mchango
mkubwa wa NMB na wadhamini wenza, nakiri kwamba kama sio nyie, hili
lisingewezekana kwa kiwango hiki.
“Tumehakikishiwa udhamini endelevu, niwaambie mnachofanya ni kusapoti jitihada za
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo inathamini michezo na uthibitisho ni
nguvu zake katika michezo yote, ikiwemo Gofu, ambako inajenga uwanja mkubwa jijini
Dodoma,” alisema Jenerali Mkunda na kuahidi kuyatumia NMB CDF Trophy kama


mazoezi kuelekea Mashindano ya Gofu ya Majeshi ya Dunia, huko San Diego,
Marekani baadaye mwaka huu
Kwa upande wake, Jenerali Nundwe akiwakilishwa na Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Henry
Odilo kutoa neno la shukrani, alisema CDF Trophy yamekuwa mashindano makubwa,
yenye mvuto na ushindani kutokana na Uratibu mzuri wa TPDF Lugalo Golf Club, zaidi
ni kwa sababu ya nguvu ya udhamini mnono wa NMB unaowapa hamasa washiriki kiasi
cha kuwa na ushindani mkubwa katika kategori zote.
“Pongezi kwa Waratibu Klabu ya Gofu Lugalo chini ya Mwenyekiti Michael Luwongo na
JWTZ kwa ujumla sio tu kwa kuandaa mashindano haya makubwa, bali kutupa nafasi
ya sisi kushiriki na aina ya mapokezi tuliyopewa na kuoneshwa kwa siku zote za kuwa
hapa.
“Tunawapongeza wadhamini NMB kwa kuipa CDF Trophy thamani kubwa, tunaamini
wataendelea kuyadhamini na Gofu Lugalo watazingatia ushiriki wetu kila mwaka, kama
ambavyo nasi tutawaalika JWTZ katika mshindano yetu yatakayofanyika Novemba
mwaka huu jijini Lilongwe, Malawi,” alisema Jenerali Mstaafu Odilo.
Awali, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi,
aliwapongeza waandaaji wa CDF Trophy, washindi wa mwaka huu na washiriki wote
kwa ujumla, huku akiihakikishia JWTZ kwamba benki yake itaendelea kuyadhamini
mashindano hayo kwa miaka mingi zaidi ijayo, kwani inathamini ushirikiano uliopo baina
yao na ndio siri ya kusaidia harakati mbalimbali za kimichezo za Majeshi ya Ulinzi na
Usalama nchini.
“Tumedhamimi CDF Trophy kwa miaka nane sasa mfululizo, ahadi yetu kwenu Klabu
ya Gofu Lugalo na JWTZ kwa ujumla, tutegemeeni sana sio tu katika suala zima la
udhamini wa shindano hili, bali ufadhili wa timu za Majeshi yetu yanapojiandaa na
Mashindano ya Majeshi kwa michezo yote, ikiwemo gofu, ngumi, mieleka, riadha, soka
na mingineyo ya kitaifa na kimataifa kama ile ya Nairobi, Kenya na Wuhan, China.
“NMB ni mdau mkubwa wa JWTZ, taasisi ambayo Ina wateja wetu wengi na hiyo ndio
siri ya kujitoa kwetu kuwezesha shughuli za kimichezo majeshini. Tunawahakikishia pia
huduma bora na rafiki kwa ajili yenu, zinazotolewa kwenye matawi yote, yakiwemo
matawi maalum ya Mlimani City, Tegeta, Ohio na Oyster Plaza,” alisema huku
alizitambulisha bidhaa mbili mpya za Akiba Plus na Wezesha Account.
Kwa upande wa matokeo, Michael Massawe aliibuka mshindi wa jumla wa CDF Trophy
2023, huku Abdallah Yusuf akitwaa taji upande wa wachezaji wa kulipwa ‘professional,’
wakati Abdallah Gunda wa NMB akiibuka bingwa wa mataji mawili katika ‘Sponsors
Category,’ na ‘Division C’. Naye Sigfrid Urassa wa NMB, pia aliibuka na vikombe viwili
vya ‘Men’s Smart Golfers’ na mshindi wa pili ‘Sponsors Category’.
Baadhi ya washindi wengine na kategori zao kwenye mabano ni: Amina Khamis
(Combat Fiddle – ladies), David Mziray (Combat Fiddle – men’s), Private Lawrence

Sangawe (Division B), Vicky Elias (Ladies), Mtei Mwamapala (men’s longest drivers),
Loveness Konky (ladies longest drivers) na Prosper Emmanuel (Division A).