Thursday, December 7, 2023
HomeTop NewsNMB yashinda tena tuzo ya kuongoza kuwafadhili wajasiriamali

NMB yashinda tena tuzo ya kuongoza kuwafadhili wajasiriamali

Na Mwandishi Wetu

Benki ya NMB imetunukiwa tena tuzo na jukwaa la kufadhili ujasiriamali
duniani (SME Finance Forum) kutokana na huduma zake wezeshi na ufadhili
wake wa kuendeleza biashara za wafanyabiashara wadogo na wakati nchini.

Ushindi iliyoupata benki hiyo kwenye tuzo za mwaka huu za ufadhili wa
ujasiriamali duniani (Global Finance Awards 2023 – GSMEFF 2023) ni wa
Mfadhili wa Ujasiriamali wa Mwaka upande wa Afrika uliyoipa tuzo ya fedha.

Washindi wa tuzo za mwaka huu walitangazwa wakati wa mkutano wa jukwaa
hilo uliofanyika kati ya Septemba 12 na 14 huko Mumbai, India.

Kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake, tuzo za GSMEFF 2023 zinatambua
dhamira na mafanikio ya taasisi za fedha na kampuni zinazojihusisha na
teknolojia za huduma za kifedha (fintech) katika kuwahudumia wateja wao
ambao ni wajasiriamali wadogo na wakati.

Ujumbe wa kauli mbiu ya tuzo za mwaka huu, ambayo ni “Mifumo ya Kidijitali
na Mustakabali wa Ufadhili wa SMEs,” uliendana na dhamira ya NMB ya
kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wakati kwani ulizingatia jinsi mifumo ya
kidijitali inavyogusa mabadiliko ya ukuaji wa uchumi duniani.

Akizungumzia ushindi wa tuzo ya mwaka huu, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB,
Bi Ruth Zaipuna, amesema heshima hiyo ni ushahidi mwingine wa juhudi za
dhati za benki hiyo za kuziba pengo la kuwafadhili wajasiriamali nchini.

“Tuzo hii kimsingi inathamini mchango na ushiriki wa benki yetu katika
kuwafadhili wajasiriamali na uwekezaji inaoufanya katika uvumbuzi wa
kidijitali,” aliongeza.

NMB inazingatia maendeleo ya wafanyabiashara haa kutokana na mchango
wao mkubwa katika ujenzi wa taifa kwa kutengeneza ajira, kuchochea ukuaji
wa uchumi na kuimarisha mapato ya wananchi.

“Tuzo hizi na heshima tuliyopata ni ushahidi wa mwendelezo wa ubora wa
huduma zetu na dhamira ya dhati ya ubunifu ya NMB,” Bi Zaipuna alisema
katika taarifa ya kuutangazia umma mafanikio hayo.

Huu ukiwa mwaka wake wa sita, tuzo za ufadhili wa ujasiriamali zilianzishwa
mwaka 2018 na SME Finance Forum ambao ni mtandao wa taasisi za fedha
wa kusaidia kuzikwamua kifedha biashara ndogo na za kati duniani.

Katika pongezi zake kwa washindi, Afisa Mtendaji Mkuu wake, Bw Matthew
Gamser, alisema ushindani wa mwaka huu ulikuwa mkubwa kutokana na
washiriki kuwa wengi wakitoka katika nchi nyingi ikilinganishwa na miaka ya
nyuma.

Kwa upande wake, mtu anayetarajiwa kumrithi, Bw Qamar Saleem, alisema
kuwafadhili wajasiriamali ni zaidi ya kuwasaidia kifedha kwani kufanya hivyo
pia kunabadilisha maisha ya watu wengi.

SME Finance Forum, inayoratibiwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) la
Benki ya Dunia, ilianzishwa mwaka 2012 na nchi 20 tajiri duniani (G20) chini
ya mwamvuli wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ujumuishaji wa Kifedha (GPFI).

Majukumu yake makubwa ni pamoja na kusimamia wanachama wake
kubadilishana maarifa, kuchochea ubunifu na kukuza ukuaji wa wajasiriamali.

RELATED ARTICLES

Most Popular