Saturday, September 14, 2024
HomeTop NewsNMB, MCL wazindua Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kidigitali

NMB, MCL wazindua Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kidigitali

NA MWANDISHI WETU
 
Benki ya NMB na Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), wamezindua
Jukwaa la Wanawake Mtandaoni ‘Rising Woman Network, lenye lengo la
kuwawezesha, kuwaendeleza na kubadili tawsira za wafanyabiashara, wajasiriamali na
wataalam wanawake nchini.
 
Uzinduzi huo ambao ni zao la ‘The Citizen Rising Woman’ iliyokuwa ikiendeshwa na
gazeti la The Citizen, umefanyika leo jijini Dar es Salaam, ambako Mkurugenzi Mtendaji
wa MCL, Bakar Machumu na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna,
walisaini hati za ushirikiano huo.
 
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa MCL, NMB
na Viongozi wanawake wa taasisi binafsi, Bi. Zaipuna alisema benki yake inaamini
katika ushirikiano na ndio siri ya uwepo wa makubaliano mengi ya mashirikiano
hususani ya kidigitali na taasisi mbalimbali nchini, kwani inaamini hiyo ndio njia kuu na
ya haraka kuifikia jamii ambayo ndio wawezeshaji wao.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kulia) akibadilishana nakala za makubaliano ya ushirikiano wa Jukwaa la “Rising Woman Online” na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Bakari Machumu (wapili kushoto), wakati wa uzinduzi wa Jukwaa hilo lenye lengo la kuwawezesha na kuwaendeleza wanawake wajasiriamali, wafanyabiashara na wafanyakazi. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Digitali wa kampuni ya Mwananchi, Happiness Watimanywa na kulia ni Mkuu wa Idara ya Bidhaa wa Benki ya NMB, Aloyse Maro. (Na Mpiga Picha Wetu).

 
Alibainisha ya kwamba NMB haitosita kuunga mkono jitihada zozote zinazolenga
kurahisisha utendaji na uendeshaji wa shughuli za wadau wao, hasa wanapogundua
kuwa kufanya hivyo kutawapa fursa ya kuyafikia makundi mengi zaidi ya kijamii, kwa
haraka zaidi, kwa wepesi zaidi na kwa muda sahihi.
 
“Ndio maana Mwananchi Communications walipokuja kutuomba ushirikiano wa
kuwawezesha wanawake wa Kitanzania, hatukusita tulikubali mara moja kwa sababu
tuliona ni moja ya fursa muhimu za kuhudumia wanawake ambao ni kundi muhimu
kwetu kama benki.
 
“Tutaendelea kusapoti Mawazo Chanya yenye kuongeza thamani na kutoa
masuluhisho ya changamoto mbalimbali kwa jamii inayotuzunguka. Tunaamini jukwaa
hili litawezesha wanawake mbalimbali, wawe wafanyabiashara, wajasiriamali,
wafanyakazi na viongozi wa kada zote.
 
“Ni jukwaa ambalo litawakutanisha pamoja, kupeana ushauri na kuwawezesha kufanya
biashara. 
 
Tayari tumeambiwa tunazindua jukwaa hili tukiwa na wanawake zaidi ya 70, sisi NMB
tunaahidi kupitia Mwamvuli wa Jasiri, tutakuwa kule na fursa zetu zinazowahusu
wanawake ambazo ni sehemu ya Jasiri, zote zitapatikana huko, ikiwemo mikopo na
nafasi za kazi, tenda na nyinginezo,” alisema Bi Zaipuna na kuwakaribisha wanawake.
 Kwa upande wake, Machumu alisema, baada ya miaka mitatu ya The Citizen Rising
Woman ya kianalogi, wanajisikia fahari kubwa kupiga hatua na kuiweka kidigitali chini
ya uwezeshaji wa NMB.

 
“Tulikuwa na miaka mitatu ya mafanikio, ikihusisha hadithi zaidi ya 200 kutoka kwa
wanawake mbalimbali nchini, na sasa tunauleta mfumo huu kidigitali, lengo likiwa
kuwajengea ujuzi na maarifa muhimu wanawake kufanikiwa katika uongozi na
usimamizi wa shughuli zao katika taasisi za umma na binafsi.
 
“Kwa kufanya hivyo, tunaamini Rising Woman network inaenda kuharakisha ukuaji na
ustawi wa kibiashara na kiuchumi, sambamba na utambuzi wa fursa zinazo wazunguka
wanawake, sanjari na kuchochea ari ya uongozi kwa kundi hili kubwa kwa jamii.
 
“Tunaishukuru NMB kwa kukubali kuungana nasi kuhuisha wazo hili ambalo huenda
lingekwama. Huu ni ushirikiano wa kimkakati unaoifanya NMB kuwa mshirika pekee
miongoni mwa taasisi za fedha nchini, wakiunagan nasi kupitia bidhaa yao ya NMB
Mwanamke Jasiri,” alibainisha Machumu.
 
Aliongeza ya kwamba, ushirikiano huo ambao unathibitisha dhamira ya pamoja ya MCL
na NMB katika kukuza viongozi na uwezeshaji wanawake nchini, huku akizitaja sifa kuu
za jukwaa hilo kuwa ni pamoja na ushirikiano na jamii, fursa za biashara na uwezeshaji
kifedha. 
 
Jukwaa hilo pia limebeba dhima ya kuelimisha, kutambua, kusherehekea na kukuza
utamaduni wa uongozi kwa wanawake na uwezeshaji kifedha mtandaoni, yote hayo
yakitarajiwa kufanyika chini ya Kaulimbiu isemayo; Wezesha Uhusiano Wake; Kukuza
Uongozi na Kuimarisha Ushirikiano.

RELATED ARTICLES

Most Popular